Dodoma inavyomaliza mwaka na huduma ya kupandikiza mimba

Published by Fadhili Paulo on

Huduma ya kupandikiza mimba Tanzania

Dodoma inavyomaliza mwaka na huduma ya kupandikiza mimba

Dodoma.

Zikiwa zimebaki siku chache kufunga mwaka wa 2021, ndoto ya Tanzania kuanza kutoa huduma ya kupandikiza mimba kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi imeanza kuonekana kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Hospitali hiyo ilianzishwa 2015 kwa tamko la Rais wa nne, Jakaya Kikwete na ilizinduliwa rasmi Oktoba 13, 2015 na imefanikiwa kuwa hospitali yenye huduma zote za kibingwa na baadhi ya huduma za ubingwa bobevu ikiwamo kupandikiza figo.

Hospitali hiyo sasa imeanza kupandikiza mimba kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi.

Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika katika taarifa yake wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wakurugenzi wa hospitali hiyo agusia maendeleo waliyofikia

“Menejimenti imekusudia kuanzisha huduma nyingine za ubingwa bobevu kama vile upandikizaji wa uroto (Bone Marrow Transplant), upandikizaji wa mimba (IVF) na matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi.”

Hata hivyo, kauli yake hiyo ilifafanuliwa zaidi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Dk Dorothy Gwajima aliyesema amekuwa akisumbuliwa kwa kupigiwa simu nyingi na wanawake wenye matatizo ya uzazi wakitaka kujua namna Serikali itakavyosaidia kuondoa tatizo hilo.

“Nimekuwa nikipigiwa simu nyingi na wenye matatizo ya uzazi kwa kuwa gharama za kupandikiza mimba kwenye hospitali binafsi gharama zake ziko juu.

“Anna uko wapi hebu njoo hapa,” Dk Gwajima alimuita Dk Anna Kasililika ambaye ni daktari wa mifumo ya uzazi anayeshughulikia kitengo cha matibabu ya uzazi ili atoe maelezo kwenye hadhara iliyofanyika kwenye eneo la Hospitali ya Benjamin Mkapa katikati ya Novemba, 2021.

Kuonyesha kwamba mwaka 2021 unaisha kwa matumaini na mwaka ujao unaanza kwa mafanikio, Dk Kasililika aliyesomea utaalamu huo kutoka Chuo Kikuu cha Pan African cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika mwaka 2019, anasema waliishaanza majaribio, lakini wanatarajia kuanza rasmi Januari mwakani.

“Tulianza kupandikiza mimba kwa mtu mmoja, lakini bahati mbaya ujauzito ulitoka,” alisema Dk Kasililika.

Anna anasema wanachofanya ni kupandikiza mbegu za kiume kwenda kwenye kizazi cha mwanamke mwenye matatizo ya uzazi.

Hata hivyo, Dk Chandika anasema maandalizi ya vitanda 400 kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ya upandikizaji mimba yameanza na Januari, 2022 yatakuwa yamekamilika.

Tamko la Wizara ya afya

Wakati akiwasilisha bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Dk Gwajima alisema Serikali inatarajia kuanza kutoa huduma ya upandikizaji wa mimba kwa kitaalamu ni ‘In Vitro Fertilization’ (IVF) kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22.

Huduma hiyo inaanza ikiwa ni miaka kadhaa imepita tangu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuanza maandalizi ya utoaji wa huduma hiyo ikiwemo kusomesha wataalamu na kuandaa jengo litakalotumika kutolea huduma hiyo.

Hata hivyo, miaka miwili tangu kuanza kwa maandalizi ya upandikizaji mimba MNH, yameibuka matatizo matano ya wanaume ambayo ndiyo chanzo cha ugumba, huku asilimia 50 ya wagumba wakiwa ni jinsi hiyo.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokuwa kabisa na mbegu, kuwa nazo zenye ubora hafifu na zisizo na mbio, mbegu chache na zinazorudi kinyumenyume au kufanya tendo mara kwa mara na hivyo kuathiri uzalishaji mbegu bora.

Gharama za upandikizaji mimba

Hata hivyo, mwaka 2019 wakati wanatambulisha uwepo wa huduma hiyo, kitengo cha magonjwa ya kinamama kilisema gharama zitakuwa ni kati ya Sh milioni 2 mpaka milioni 10, kulingana na ukubwa wa tatizo.

Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa hospitali kadhaa zinazopandikiza mimba nchini na nje ya nchi hutoza kati ya Sh milioni 8 mpaka Sh milioni 25.

Upandikizaji mimba

Akinukuliwa na gazeti hili hivi karibuni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Vincent Tarimo wa hospitali ya Muhimbili alisema kuanzishwa kwa huduma ya upandikizaji mimba imetokana na idadi kubwa ya wanandoa wanaohitaji usaidizi wa kupata watoto, baada ya via vya uzazi kwa wanawake kuharibika huku wanaume wakiwa na mbegu zisizo na uwezo wa kusafiri haraka kulifikia yai lililorutubishwa.

Alisema tatizo hilo linaongezeka kwa sasa kwani kitakwimu Muhimbili inahudumia wanawake wapatao 1,200 kwa mwaka, ambao wana tatizo la kutopata ujauzito na suluhu ni kuwapandikiza mimba.

Dk Tarimo alisema tatizo la mama kushindwa kupata mtoto lipo na linaongezeka kila siku huku akitaja chanzo ni hutokana na mirija yake kuwa na matatizo na inawezekana imeharibiwa na maambukizi kwenye mirija ya uzazi kwa kuharibiwa na wadudu.

“Kwa wastani mimi nikiwa kliniki huwa nahudumia mara moja kwa wiki kwa magonjwa yanayohusisha uzazi isipokuwa ujauzito, naona wagonjwa watano kwa siku wenye tatizo la ugumba,” alisema Dk Tarimo na kuongeza:

“Naweza kuona watano kwa hivyo kwa wastani kwa wiki Hospitali ya Muhimbili inaona wagonjwa si chini ya 25 na kwa mwezi tunaona wagonjwa 100, tunahesabu kwa mwaka ni 1,200.”

Alisema wanawake wanaweza kusaidiwa na kupandikizwa kwa kuruka njia ya asili tangu yai linapotoka kuweza kupita kwenye mirija mpaka kwenye mji wa mimba, kulivuna moja kwa moja likishakuwa tayari baada ya hapo anamsaidia kulipandikiza ndani ya kizazi chake hivyo, halipiti tena kwenye njia yake ya kawaida.

Hata hivyo, Dk Tarimo alisema tatizo hilo linachangiwa na pande mbili; mwanamke na mwanaume ingawa kwa Watanzania na Waafrika wengi lawama zinakwenda kwa mwanamke ambaye ndiye anabeba ujauzito.

“Unaweza kukuta huyu baba ana matatizo yanayomfanya ashindwe kupata mtoto kwa hiyo naye anaweza akasaidiwa kwa huduma kama uwezo wake ni mdogo. Kama shida anayo mwanamke peke yake ni mirija siyo mwanaume hiyo ni rahisi sana kufanyika,” alisema Dk Tarimo na kuongeza:

“Kwa kuwa utavuna yai la baba na mama kuna dawa utampa ya kustimulate (kuchochea) halafu unavuna yai la mama utaweka kwenye kifaa maalumu incubater halafu utampandikizia mama.”

Alisema ikiwa baba na mama kwa pamoja wana shida hasa baba idadi yake ya mbegu ni ndogo, tiba hiyo itatakiwa kuchagua yai lenye ubora au mbegu ndilo litakaloweza kutoa mtoto.

“Kuna idadi ya mbegu za baba inabidi uwe nayo ndiyo uweze kupata mtoto kuna zile zinazokwenda kwa kasi zifike mapema na kurutubisha yai la mama, kama hazipo zenye kasi au zipo chache basi kwa kutumia utaratibu huu unaweza kuchagua ambazo ni nzuri na ukazitumia kama baba unakuta mayai yake machache sana au mengi hayana kasi, kwa sababu mama huwa anatoa yai moja tu lakini baba huwa anatoa mengi kwa hiyo hapo unachagua linalofaa,” alisema.

Chanzo cha tatizo

Dk Tarimo alisema maisha yanachangia kwa kiwango kikubwa kuleta tatizo la ugumba kwa pande zote mbili.

“Wasichana wanaanza tendo la ndoa mapema kwa hivyo unakuta labda alianza tangu shule ya msingi, hivyo inamuongezea hatari ya kupata maambukizi katika via vya uzazi kwa hiyo unakuta ikiathiri mfumo wa uzazi inasababisha ugumba.

Pia, alitaja sababu za wanaume kukumbwa na tatizo la ugumba. “Wengi kutokula vizuri, mwili hautumiki sana na tunakula vyakula ambavyo havina lishe na virutubisho kwa mtu kutoa mayai ambayo yana ubora, ulevi na mazingira ambayo joto ni kubwa, hivyo inaathiri uzalishaji wa mbegu na wengine wanatumia sigara, bangi vyote vinaathiri uzalishaji wa mbegu bora za kiume.”

Sehemu nyingine duniani

Huduma hiyo ya kitabibu imekuwa ikitumika sehemu mbalimbali duniani kwa miongo minne sasa na katika miaka ya hivi karibuni imezidi kusogezwa katika hospitali za umma katika maeneo ambayo wananchi wake hawana uwezo wa kuipata huduma hiyo katika hospitali binafsi.

Mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa kutumia njia ya upandikizaji wa mimba ni Louise Brown aliyezaliwa nchini Uingereza.

source


2 Comments

Esther Mathayo Lupande · 10/05/2022 at 9:16 pm

Ninahitaji huduma ya kupanfikiza

    Fadhili Paulo · 15/05/2022 at 5:51 am

    Wasiliana na wahusika kama niliyoeleza kwenye makala kwamba ni hospitali ya Dodoma kwa kushirikiana na hospitali ya Taifa mhimbili

Leave a Reply

Avatar placeholder

Your email address will not be published.

WhatsApp WhatsApp +255714800175