Wanawake 500 wapata mimba kwa upandikizaji Arusha

Published by Fadhili Paulo on

Wanawake 500 wapata mimba kwa upandikizaji Arusha.

Mwanamke mmoja (50), amefanikiwa kupata watoto mapacha kwa njia ya upandikizaji mimba jijini Arusha.

Mwanamama huyo ni mmoja kati ya wanawake 500 waliofanikiwa kupata watoto kwa huduma hiyo inayotolewa na kituo cha Huduma ya Uzazi na Upandikizaji Mimba cha Avinta Care Medical kilichopo jijini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mapema wikii hii, Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa kituo hicho, Nicholaus Mazuguni amesema kwa sasa wanafanya huduma hiyo wakishirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Amesema waliamua kutoa huduma hiyo ili kutatua changamoto ya uzazi iliyokuwa ikisumbua familia nyingi na kufuata huduma hiyo nje ya nchi, ambapo kwa sasa wanahudumia wagonjwa 100 kwa wiki.

“Tumeanza kutoa huduma hii 2017, tumeshapandikiza wanawake zaidi ya 500 na kufanikiwa kupata watoto zaidi ya 250. Mwitikio ni mkubwa kwa sababu watu walikuwa wanatumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi”

“Mara ya mwisho tumempandikiza mapacha mwanamke mwenye miaka 50 na amefanikiwa kupata watoto wake vizuri bila shida yoyote. Wengi wanafurahi kwani wameteseka na kukutana na changamoto nyingi katika kutafuta watoto. Gharama zetu za utoaji wa huduma ni kuanzia Sh7 milioni na kuendelea kulingana na umri wa mgonjwa”amesema.

Kwa upande wake Daktari wa akinamama kutokana Muhimbili, Hildegarda Aloyce amesema wamekuwa wakishirikiana na kituo hicho cha Avinta katika kutatua changamoto za uzazi kwani tatizo hilo bado ni kubwa katika jamii ambapo kati ya wagonjwa 10 ambao wamekuwa wakipokelewa wagonjwa 4 hadi 6 wana tatizo la uzazi .

Mganga Mkuu wa mkoa ,Dokta Sylvia Mamkwe amepongeza juhudi hizo zilizofanywa na kituo hicho kwa kushirikiana na hospitali nyingine,na Kama serikali wapo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha huduma hiyo ili kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi.

Mmoja wa wanufaika kutokaa wilayani Simanjiro, Martha Sangwa amesema kuwa, amefurahishwa Sana kwa huduma hiyo iliyomfanikisha kupata watoto mapacha kwani ameteseka kwa miaka 16 bila msaada wowote,hivyo uwepo wa kituo hicho ni faraja kubwa Sana kwao na kuwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.

Source : Mwananchi

(Visited 128 times, 1 visits today)

0 Comments

Leave a Reply

Avatar placeholder

Your email address will not be published.

WhatsApp WhatsApp +255714800175